Kongo yataka msemaji wa MONUSCO kufukuzwa nchini humo – DW – 03.08.2022
  1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yataka msemaji wa MONUSCO kufukuzwa nchini humo

3 Agosti 2022

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeutaka ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, kumfukuza msemaji wake Mathias Gillman kutoka nchini humo, haraka iwezekanavyo.

https://p.dw.com/p/4F4Bk
Demokratische Republik Kongo | Proteste in Goma gegen UN Mission MONUSCO
Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Hii ni kutokana na kauli aliyoitoa, iliyotajwa kuwa yenye madhara yasiyofutika na yasiyo sahihi.

Hayo yanajiri wakati Kinshasa ikitangaza kutatathmini upya mpango wa kuwaondoa askari wa MONUSCO kufuatia maandamano ya vurugu wiki iliyopita, na kuashiria uwezekano wa kuwalazimisha wafanyakazi wa ujumbe huo kuondoka mapema kuliko ilivyotarajiwa.

Kupitia taarifa, serikali iliagiza hapo jana  kufanyika mkutano na MONUSCO ili kujadili mpango wake wa kuondoka nchini humo. Kongo imesema raia 29 na wanajeshi wanne wa MONUSCO waliuawa wakati wa maandamano yaliyotokea mashariki mwa nchi hiyo.

Waandamanaji walikuwa wanashinikiza askari hao kuondoka kwa kushindwa kuwalinda raia dhidi ya mashambulizi ya makundi ya waasi.