Tunachofahamu kuhusu shambulio la Israel dhidi ya Iran

.

Chanzo cha picha, EPA

Maafisa wa Marekani wanasema Israel iliipiga Iran kwa kombora usiku wa kuamkia leo, katika kile kinachoonekana kuwa ni shambulio la kulipiza kisasi baada ya majuma kadhaa ya mvutano unaoongezeka kati ya nchi hizo mbili.

Kuna madai yanayoshindana kuhusu ukubwa wa shambulio katika eneo la Isfahan na kiwango cha uharibifu, huku vyombo vya habari vya Iran vikipuuza umuhimu wake.

Inakuja baada ya wiki kadhaa za mvutano unaoongezeka kati ya wapinzani wa kikanda, ambao tayari wameshuhudia shambulio la Israeli kwenye ubalozi wa Iran huko Syria, na Iran kuanzisha shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa dhidi ya Israeli.

Hapa kuna kila kitu tunachojua kuhusu tukio la hivi punde hadi sasa.

Tunajuaje kuwa kumekuwa na shambulio?

Israel haikiri mara kwa mara hatua zake za kijeshi, ambazo zimelenga makundi yenye silaha yanayoungwa mkono na Iran nchini Syria na Iraq mara nyingi.

Hata hivyo, maafisa wa Marekani wameithibitishia mshirika wa BBC, CBS News kwamba kombora la Israel liliipiga Iran mapema siku ya Ijumaa. Kuna uwezekano mkubwa Marekani ingeambiwa kuhusu mipango hiyo mapema.

Haijulikani ni aina gani ya silaha zilitumika au zilirushwa kutoka wapi.

Duru za Marekani zilisema kuwa kombora lilihusika katika shambulio hilo, huku Iran ikisema kuwa lilihusisha ndege ndogo zisizo na rubani.

Serikali ya Iran inadhibiti vikali ufikiaji wa nchi hiyo. BBC haina ufikiaji wa moja kwa moja katika eneo la kati la Isfahan, ambapo tukio hili lilitokea.

Iran inasema nini kuhusu shambulio hilo?

Maafisa wa Iran na vyombo vya habari vimethibitisha kuwa kulikuwa na jaribio la shambulio lakini wanapuuza umuhimu wake. Hakujawa na ripoti za majeruhi.

Shirika la habari la Iran la Fars limesema milipuko ilisikika karibu na kambi ya jeshi na mifumo ya ulinzi wa anga iliwashwa.

Kituo cha habari cha serikali kilimnukuu jenerali mmoja huko Isfahan akisema milipuko iliyosikika katika eneo hilo "ilitokana na ulinzi wa anga kufyatua vitu vya kutiliwa shaka", na kusema hakukuwa na uharibifu wowote.

.

Chanzo cha picha, IRIB

Shirika la habari la Iran la Tasnim, ambalo liko karibu na tawi la kijeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran, lilichapisha video ya kituo cha nyuklia huko Isfahan ambacho hakikuonyesha dalili zozote kuwa kimepigwa.

Shirika la Kimataifa wa Nishati ya Atomiki limethibitisha kuwa hakuna uharibifu wowote katika maeneo ya nyuklia ya Iran.

Hossein Dalirian, msemaji wa Kituo cha Kitaifa cha Mtandao cha Iran, alisema "hakuna shambulio la anga kutoka nje ya mipaka".

Alisema Israel "ilifanya tu jaribio lisilofanikiwa na la kufedhehesha la kurusha ndege zisizokuwa na rubani lakini pia zimedunguliwa".

Iran iliweka mafuku kwa safari za ndege za kibiashara saa chache baada ya shambulio lakini sasa vimeondolewa.

Milipuko pia iliripotiwa nchini Iraq na Syria - ambapo makundi yenye silaha yanayoungwa mkono na Iran yanaendesha shughuli zake - usiku kucha, lakini haijulikani ikiwa yanahusishwa moja kwa moja na shambulio la Isfahan.

Wizara ya ulinzi ya Syria imesema eneo la ulinzi wa anga kusini mwa Syria lilipigwa na kombora la Israel mapema asubuhi ya Ijumaa saa za huko. Israel haijathibitisha kuhusika na shambulio hilo.

Kwa nini Isfahan alilengwa na kwa nini ni sasa?

Mkoa wa Isfahan ni eneo kubwa katikati mwa Iran ambalo lilichukua jina lake kutoka kwa mji wake mkubwa zaidi.

Eneo hilo ni nyumbani kwa miundombinu muhimu ya kijeshi ya Iran, ikiwa ni pamoja na kambi kubwa ya anga, eneo kubwa la uzalishaji wa makombora na vituo kadhaa vya nyuklia.

Shambulio hili la hivi punde linakuja chini ya wiki moja baada ya Iran kurusha mamia ya makombora na ndege zisizo na rubani huko Israel, tukio ambalo linaonekana kama kuongezeka kwa hali ya wasiwasi.

Licha ya ukubwa wake na hali isiyokuwa ya kawaida, shambulio la Iran kwa kiasi kikubwa halikufaulu, huku makombora mengi yakidunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga wa Israel kwa usaidizi wa Marekani, Uingereza na washirika wengine.

Shambulio hilo ambalo halijawahi kushuhudiwa katika ardhi ya Israel lilikuwa ni kujibu shambulio dhidi ya jengo kwenye jumba la wanadiplomasia wa Iran nchini Syria tarehe 1 Aprili.

Israel haijathibitisha hadharani kuwa ilihusika kwenye shambulio hilo, lakini inakubaliwa na wengi kwamba ilihusika.

Je, hii itaongeza mvutano kati ya Israel na Iran?

.

Chanzo cha picha, EPA

Umuhimu kamili wa shambulio hili la punde bado unadhihirika na bado haijajulikana iwapo Iran itajaribu kujibu.

Mwandishi wa usalama wa BBC Frank Gardener alielezea ukubwa wa shambulio la Ijumaa kama "kidogo, kama ishara", na limebuniwa kuhakikisha mzozo hauendelei zaidi.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atakabiliwa na shinikizo pinzani kutoka kwa baadhi ya majenerali wake na washirika wake wa kisiasa kuchukua hatua dhidi ya Iran, kulingana na mhariri wa kimataifa wa BBC Jeremy Bowen.

Israel imekuwa chini ya shinikizo kubwa la kimataifa kutoka kwa Marekani na washirika wengine wa magharibi kuitaka isichukue hatua yoyote ambayo itageuza mzozo wa muda mrefu kati ya wapinzani hao wawili wa Mashariki ya Kati kuwa vita vya moja kwa moja.

Kupamba moto huku kwa uhasama kunakuja huku kukiwa na vita huko Gaza, ambapo jeshi la Israel linapambana na Hamas inayoungwa mkono na Iran.

Je, uchumi wa dunia umechukua hatua gani?

Kuna wasiwasi kwamba mzozo unaozidi kuwa mbaya katika Mashariki ya Kati unaweza kuvuruga usambazaji wa mafuta.

Brent crude, kigezo cha kimataifa cha bei ya mafuta, kilipanda kwa 1.8% hadi $88 kwa pipa baada ya shambulio hilo.

Bei ya mafuta ilikuwa imepanda kwa asilimia 3.5 hapo awali lakini ilitulia ilipobainika kuwa shambulio hilo lilikuwa kidogo.

Bei ya dhahabu - ambayo mara nyingi huonekana kama uwekezaji salama wakati wa ukosefu wa uhakika - ilikaribia kwa ufupi rekodi ya juu kabla ya kushuka hadi karibu dola 2,400 kwa aunzi.