Kampeni ya 'Wekeza NBC Shambani Ushinde’, yahitimishwa, mshindi apewa trekta | Nipashe

Kampeni ya 'Wekeza NBC Shambani Ushinde’, yahitimishwa, mshindi apewa trekta

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:54 AM May 15 2024
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Lindi Majid Myao (alieketi kwenye trekta) akijaribu ubora wa trekta lililotolewa na benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao baada ya chama hicho kuibuka mshindi wa kampeni hiyo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Lindi Majid Myao (alieketi kwenye trekta) akijaribu ubora wa trekta lililotolewa na benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao baada ya chama hicho kuibuka mshindi wa kampeni hiyo.

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imehitimisha msimu wa tatu wa kampeni yake ya 'Wekeza NBC Shambani Ushinde’ maalum kwa wakulima wa zao la korosho katika mikoa ya Mtwara na Lindi kwa kukabidhi zawadi kuu ya trekta kwa mshindi mkubwa wa kampeni hiyo ambae ni Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao.

Kampeni hiyo iliyozinduliwa mwezi Oktoba mwaka jana mkoani Mtwara ililenga kuchochea kiwango cha uzalishaji wa zao la korosho na mazao mengine katika mikoa hiyo ikihusisha zawadi mbalimbali kwa washindi zikiwemo Simu janja ‘Smartphone’, Pampu za Kupulizia dawa, TV, Pikipiki, kompyuta mpakato ‘laptop’, Mizani za kidijitali na trekta.

Hafla ya makabidhiano ya zawadi hiyo yamefanyika mwishoni mwa wiki kwenye ofisi za  Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao mkoani Lindi yakienda sambamba na Mkutano Mkuu wa saba wa chama hicho. Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Lindi Majid Myao aliongoza hafla hiyo iliyohusisha viongozi na wanachama wa chama hicho huku Meneja wa Benki ya NBC tawi la Lindi, Iovin Mapunda akiowaongoza maofisa wengine wa benki hiyo kwenye hafla hiyo.

 Akizungumza kwenye hafla hiyo Myao alisema zawadi hizo zimekuja wakati mwafaka kwa kuwa mkoa huo kwasasa unatekeleza mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la korosho ili kwenda sambamba na azma ya serikali ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo hadi kufikia tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.

“Ni mpango wa serikali kuona sekta ya kilimo inakua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, hivyo tunashukuru kuona benki ya NBC inashiriki kikamilifu katika kufanikisha azma hiyo kupitia 'Wekeza NBC Shambani Ushinde.’‘’ Alisema Myao  huku akiwaomba wataalamu wa kilimo mkoani humo kuwatembelea wakulima mara kwa mara ili kuwapa elimu itakayowawezesha kuzalisha korosho bora.

Aidha alisisitiza wakulima wa mkoa huo kuhakikisha wanahifadhi fedha zao benki pamoja na kuwa na nidhamu ya fedha ikiwa ni pamoja na kuwekeza zaidi kwenye ununuzi wa vifaa vya kilimo cha kisasa ili kuongeza uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.

 

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mapunda alisema tangu kuanza kwa kampeni hiyo, jumla ya washindi 150 wakiwemo wakulima mmoja mmoja, vyama vya msingi (AMCOS) na vyama vikuu vya ushirika kutoka mikoa ya Lindi na Mtwara. Washindi hao walipata zawadi mbalimbali zenye jumla ya thamani ya sh 200 Milioni.

"Tukiwa tunatarajia kuzindua msimu wa nne wa kampeni hii mwishoni mwa wiki hii naendelea kutoa wito  kwa wakulima kuendelea kupitisha fedha zao za malipo ya korosho kupitia akaunti zao za 'NBC Shambani' ili kupata fursa ya kufurahia zaidi manufaa yatokanayo na akaunti hiyo. " alisema.

Aidha, Mapunda alisisitiza kuwa benki hiyo imedhamiria kushirikiana vyema na wakulima ili kuhakikisha wanaboresha sekta ya kilimo na kwamba mbali na kampeni hiyo ya 'Wekeza NBC Shambani Ushinde’ benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo tofauti kwa vyama vya msingi mbalimbali katika mikoa hiyo ikiwa ni namna ya kusaidia utendaji kazi wao katika shughuli zinazohusiana na uzalishaji wa korosho.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Meneja Chama Cha Ushirika cha Lindi Mwambao Nurdin Swala aliishukuru benki hiyo kwa kuandaa kampeni hiyo kwa kuwa imekuwa na msaada mkubwa kwao huku akibainisha kuwa siri ya ushindi wao ni kuitumia zaidi benki hiyo katika kupitisha malipo yao yatokanayo na mauzo ya zao la korosho.

"Tunashukuru sana Benki ya NBC kwa zawadi ya trekta hili kwa kuwa itatusaidia sana kufikia malengo yetu ambayo ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa korosho mkoani Lindi. Pia tunaahidi kuendelea kuelekeza fedha zetu kupitia akaunti ya ‘NBC Shambani’ ili kujishindia zawadi nyingi zaidi msimu ujao wa kampeni hii,’ aliahidi Swala.