NBC yaja na kadi uanachama Msalaba Mwekundu, Dk.Biteko aguswa na jitihada zake | Nipashe

NBC yaja na kadi uanachama Msalaba Mwekundu, Dk.Biteko aguswa na jitihada zake

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:58 AM May 15 2024

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Dotto Biteko (wa nne kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania za benki ya NBC.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Dotto Biteko (wa nne kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania za benki ya NBC.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Dotto Biteko amepongeza jitihada za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kuunga mkono jitihada za serikali katika kuongeza ujumuifu katika huduma za kifedha (financial inclusion) sambamba na kusaidia ufanikishaji wa miradi mikubwa ya kitaifa ukiwemo ujenzi wa miundombinu ya maji Mkoani Tanga kupitia hati fungani ya kijani iliyosimamiwa na benki hiyo.

Dk. Biteko alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki alipotembelea banda la benki hiyo lililokuwa kwenye viunga vya ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma ambapo yalifanyika Maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania. Dkt Biteko alimuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassani kwenye maadhimisho hayo ambayo pia yalihusisha uzinduzi wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa chama hicho kupitia benki ya NBC.

Akizungumza mara baada kupokea taarifa ya Meneja wa Kanda ya Kati wa benki ya NBC Miraji Msuya kuhusu jitihada mbalimbali za benki hiyo katika kuhudumia jamii ukiwemo  usimamizi wa hati fungani  ya kijani ya ujenzi wa miundombinu ya maji Mkoani Tanga na utambulisho wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa chama  cha Msalaba Mwekundu, Dk. Biteko aliipongeza benki  hiyo kwa jitihada hizo huku akitoa wito kwa taasisi za fedha nchini kuendelea kushirikiana na serikali kubuni huduma mbalimbali zinazolenga kuwakwamua wananchi kwenye changamoto zinazowakabili.

“Niwapongeze sana NBC kwa jitihada hizi na wito wangu kwa taasisi za fedha ni wao kuendelea kushikirikiana na serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kutatua changamoto za wananchi kama ujenzi wa miundombinu ya maji pamoja na kuendelea kuvutia wananchi wengi zaidi waingine kwenye mfumo rasmi wa huduma za kifedha,’’ alisema.

Dk. Biteko pia aliongoza zoezi la uzinduzi wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kupitia benki ya NBC akiwa sambamba na viongozi wengine waandamizi wa serikali wakiwemo mawaziri, viongozi waandamizi wa Chama cha Msalaba wakiongozwa na Rais wa chama hicho ambae pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile pamoja na maofisa wa benki hiyo wakiongozwa na Meneja wa Kanda ya Kati wa benki ya NBC Miraji Msuya.

Akizungumzia hatua hiyo Msuya alisema ni matokeo ya ushirikiano baina ya benki hiyo na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania unaochochewa na azma ya pamoja baina ya taasisi hizo mbili ambayo ni kujitolea katika kusaidia jamii kwenye masuala mbalimbali ya kibinadamu ikiwemo utoaji wa misaada tofauti kufuatia athari  zitokanazo na majanga mbalimbali yanayolikumba taifa.

“Ni kutokana na kushabihiana kwa dhamira  baina yetu NBC na wenzetu wa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania ndio kumesababisha ushirikiano huu unaoshuhudiwa leo. Pamoja na kuwa sehemu wa wadau muhimu katika kufanikisha maadhimisho haya, leo benki ya NBC tunashirikiana na chama hiki kuzindua kazi mpya za Kielectronic za wanachama wa chama hiki ambazo pamoja na kuwa kadi za uachama wa Red Cross pia zinawawezesha kufanya miamala mbalimbali ya kibenki,’’ alisema Msuya.

Akizungumzia zaidi faida zinazoambata na kadi hiyo kwa wanachama hao, Msuya alisema zimeunganishwa na huduma ya bima ya afya kwa wanachama inayomuwezesha mwanachama kulipwa fidia akipata ulemavu au familia yake kulipwa viwango tofauti pindi muhusika anapofariki.

“Zaidi kadi hiyo inamuwezesha mwananchama kulipia ada za uanachama, kulipia malipo mbalimbali ikiwemo ikiwemo visimbuzi vya TV na  kulipia mechi za ligi Kuu ya NBC ‘’ aliongeza.