Hali DRC sasa imefikia pabaya, amani inahitajika haraka: UNICEF Chaiban | Habari za UN
Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali DRC sasa imefikia pabaya, amani inahitajika haraka: UNICEF Chaiban

Clémence Ndabohweje, mwenye umri wa miaka 49, akisafisha vyombo nje ya makazi yake kwenye kambi ya wakimbizi ya ndani ya Kanyaruchinya huko Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC kufuatia mashambulizi ya M23. Anaishi hapa yeye na watoto wake 6 na waj…
UNICEF/Arlette Bashizi
Clémence Ndabohweje, mwenye umri wa miaka 49, akisafisha vyombo nje ya makazi yake kwenye kambi ya wakimbizi ya ndani ya Kanyaruchinya huko Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC kufuatia mashambulizi ya M23. Anaishi hapa yeye na watoto wake 6 na wajukuu watatu.

Hali DRC sasa imefikia pabaya, amani inahitajika haraka: UNICEF Chaiban

Amani na Usalama

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF anayehusika na shughuli za kibinadamu na operesheni za Ugavi, Ted Chaiban, amehitimisha ziara ya siku tano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ambako alikutana na mamlaka na kujionea athari mbaya za kuongezeka kwa migogoro kwa watu walio hatarini, haswa wanawake na watoto.

Chaiban amesema "Kiwango cha mzozo wa Mashariki mwa DRC kimefikia kilele kipya, na kusababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao na kusababisha janga baya zaidi la kibinadamu nchini hapa tangu 2003. Watoto wanauawa, kulemazwa, kutekwa nyara, na kuandikishwa na vikundi vyenye silaha vinavyotekeleza ukiukwaji mkubwa zaidi uliothibitishwa, haki zao za elimu na utoto salama zimeporwa.”

Ameongeza kuwa kiwango cha juu cha sasa cha wakimbizi wa ndani milioni ambacho ni milioni 7.2 kinaweza kuongezeka zaidi huku makundi yenye silaha yakichukua udhibiti wa maeneo mengi zaidi mashariki mwa DRC na makabiliano katika ardhi ya Congo yakienea, yote hayo yanafanyika wakati huo huo kuondoka kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka amani nchini humo MONUSCO umeanza kuondoka. 

"Tunaona kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaouawa na kujeruhiwa na mabadiliko ya hivi karibuni ya matumizi ya silaha nzito na za kisasa".

Wakimbizi wa ndani Bulengo na Lushagala

Chaiban pia alitembelea makazi ya wakimbizi wa ndani ya Bulengo na Lushagala nje kidogo ya mji wa Goma, ambako ni nyumbani kwa zaidi ya familia 36,500. Akiwa hapo amesisitiza kuwa "Kuongezeka kwa mapigano katika miezi ya hivi karibuni kumezidisha hali ambayo tayari ni hatari kwa watoto na familia katika kambi kuwa mbayá zaidi".

Akiwa hapo Chaiban alikutana na familia zilizokimbia makazi yao huko Minova ambapo ufikiaji wa misaada unazidi kuwa mdogo, na ongezeko la hivi karibuni la wimbi la zaidi ya watu 250,000 wanaokimbia migogoro limeongeza shinikizo kubwa kwa jamii ambazo tayari ziko hatarini.

"Njia pekee ya kupunguza mateso haya ni kuongeza maradufu juhudi za watendaji wa kikanda na jumuiya ya kimataifa kujadili suluhisho la kisiasa la mzozo huo, ikiwa ni pamoja na mchakato wa Luanda, mazungumzo ya Nairobi na juhudi nyingine za kidiplomasia. Kuzorota kwa hali ya usalama katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri kuna athari kubwa katika utoaji wa misaada ya kibinadamu," amesema Chaiban.

Kushambulia makazi ya wakimbizi wa ndani haikubaliki

Bwana Chaiban pia amesema "Tunalaani vikali milipuko ya mabomu ya wiki iliyopita kwenye maeneo matatu kwa watu waliokimbia makazi yao katika vitongoji vya Lac-vert, Lushagala, na Mugunga karibu na Goma, ambayo yalisababisha vifo vya watu 35 na kujeruhi zaidi ya watu 20, haswa wanawake na watoto." 

UNICEF inazitaka pande zote katika mzozo kuweka vituo vyote vya kijeshi, silaha na operesheni mbali na maeneo ya kiraia.

UNICEF inathibitisha haja ya kuwa na ulinzi mkuu katika mgogoro huu. "UNICEF inasalia kujitolea kuhakikisha kwamba haki ya kila mtoto ya kupata elimu, afya, na ulinzi inazingatiwa," amesema Chaiban.

Kwa kupungua kwa ufadhili wa kibinadamu, afua za kibinadamu zinazoongozwa na UNICEF zinalenga walio hatarini zaidi. 

"Kukabiliana na kiwango kamili cha mahitaji na kuleta suluhisho la kudumu kunaweza tu kupatikana kwa serikali kuchukua jukumu la msingi la kutoa huduma za kimsingi katika mazingira haya magumu, kwa msaada wetu wa pamoja".

Ted Chaiban amesema "Msaada kwa mifumo ya serikali kwa jamii kuwa na mnepo zaidi ndiyo njia pekee ya kupunguza mahitaji ya kibinadamu", akisistiza umuhimu wa ufadhili unaobadilika kama mojawapo ya viwezeshaji muhimu. UNICEF inafanya kazi kwa karibu na shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, na lile la chakula na kilimo  FAO, na mashirika dada ili kuimarisha uthabiti na mshikamano wa kijamii, kuunganisha afua za kibinadamu, maendeleo na amani.

Ziara jimboni Rutshuru

Chaiban alitembelea mitandao ya maji katika eneo la Rutshuru, akionyesha jinsi suluhu zilivyo za kudumu za jinsi tunavyoweza na tunavyopaswa kufanya kazi, hata katika maeneo yenye migogoro na kambi za watu waliofurushwa mwakwao kama vile upanuzi wa mtandao wa maji wa Goma huko Kanyaruchinya.

Kwa mujibu wa shirika hilo dunia inahitaji Congo yenye amani na tija, ambayo pamoja na msitu wa mvua wa kitropiki na madini ya kijani kibichi, ni muhimu kwa mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi duniani. 

Kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa, Congo inaweza kuwa nchi ya Suluhu limesema shirika hilo la kuhudumia watoto.

Chaiban amemalizia kwa kusema kwamba "DRC ni kubwa sana kushindwa. Tunahitaji amani na usalama kwa watu waliofurushwa iki waweze kurejea nyumbani, kulima mashamba yao na kuwarejesha watoto wao shuleni”, 

Naibu Mkurugenzi Mtendaji huyo Ted Chaiban anahitimisha ziara yake Mashariki mwa DRC, kwa kusisitiza kuwa hali ya kibinadamu sasa iko katika hatua ya mwisho, kuna hitaji la dharura la amani na jukumu kuu la Serikali mpya.

Afisa huyo wa UNICEF aangazia wasiwasi unaoongezeka wa kulinda haki za watoto na ulinzi wa raia huku kukiwa na hali mbaya ya kibinadamu na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuimarisha suluhu za kidiplomasia na za muda mrefu mashariki mwa DRC.