Mpinzani aliyetoroka China miongo kadhaa bado anafuatiliwa

kjh
Maelezo ya picha, Beijing 1989: Yan Xiong pichani wakati wa maandamano ya Tiananmen Square
  • Author, Gordon Corera
  • Nafasi, BBC

Miongo mitatu iliyopita, wapinzani na wakosoaji wa China walikuwa wakitoroshwa nje ya nchi kwa njia ya magendo katika operesheni ya siri iitwayo Yellow Bird - lakini mmoja wao anaiambia BBC kuwa China bado inawafuatilia.

Juni 1992: Usiku wa manane kwenye Bahari ya Kusini ya China, boti ya doria ya China ilikuwa ikikaribia boti iliyokuwa ikitoka China bara na kuelekea koloni la Uingereza la Hong Kong.

Askari wa mpakani walipoingia kwenye boti kuzungumza na wafanyakazi, sauti zao zilisikika na kundi la watu waliojaa kwenye chumba cha siri cha chini ya boti.

Mmoja wa abiria waliojificha ni, Yan Xiong. Wengi wa waliojificha walikuwa wahamiaji wa kiuchumi, wakitarajia kupata kazi Hong Kong - lakini sio Yan. Alikuwa mpinzani wa kisiasa.

Boti ya doria hatimaye liliondoka, na Yan - ambaye hakuwahi kusafiri kwa boti kabla ya usiku huo - aliwasili Hong Kong.

Baada ya kifungua kinywa, alipelekwa kwenye kituo cha kizuizini. Aliambiwa, ni kwa usalama wake mwenyewe. Kutembea mitaani kunaweza kuwa hatari.

Pia unaweza kusoma

Kuwa kizuizini China

L

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Jeshi la China liliingia kukandamiza maandamano ya Tiananmen Square

Kuwa kizuizini haikuwa jambo geni kwa Yan. Tayari alikuwa amekaa kwa muda wa miezi 19 katika gereza la China baada ya maandamano ya 1989 ya Tiananmen Square. Wanafunzi waliandamana kutaka uwepo wa demokrasia na uhuru zaidi, lakini Chama cha Kikomunisti kilituma vifaru ili kuwakandamiza.

Mwishoni mwa Juni 1989, serikali ya China ilisema raia 200 na maafisa kadhaa wa usalama walifariki. Makadirio mengine yanasema waliofariki ni maelfu.

Alipoachiliwa Yan, alielekea kusini mwa China, ambako alitumia zaidi ya kibanda kimoja cha simu, ili kuwasiliana na watu ambao wangeweza kumtorosha.

Hakuwa mpinzani pekee aliyefanya safari hii ya hatari. Akizungumza na BBC, Chaohua Wang anakumbuka kutoroka kwake.

Licha ya kuwa namba 14 kwenye orodha ya watu 21 wanaosakwa zaidi baada ya maandamano ya Tiananmen Square, alifanikiwa kukwepa kukamatwa, akijificha kwenye vyumba vidogo kwa miezi kadhaa kabla ya kuelekea kusini na kuwa sehemu ya operesheni ya kutoroshwa ya Yellow Bird.

"Nilikuwa kama kifurushi kinachohamishwa kutoka [mtu] mmoja hadi mwingine," anasema.

"Sikujua hata jina la Yellow Bird kwa miaka hiyo."

Operesheni ya Yellow Bird

K
Maelezo ya picha, Yan alijaribu kugombea kiti cha Congress huko New York mnamo 2022

Yellow Bird inaweza kuonekana kama operesheni ya kawaida ya kijasusi, na wengi waliamini shirika la kijasusi la Uingereza la MI6 au CIA la Marekani - ndio lilikuwa nyuma ya wazo hilo. Lakini hapana.

Ilikuwa ni operesheni binafsi iliyofanywa na vikundi vya watu kutoka Hong Kong, wakichochewa na hamu ya kusaidia wale ambao walikuwa wakitoroka. Miongoni mwao ni watu kutoka tasnia ya filamu, burudani na wahalifu.

"Watu hao walikuwa na polisi wengi wa China mifukoni mwao," anasema Nigel Inkster, ambaye wakati huo alikuwa afisa wa ujasusi aliyeishi Hong Kong. Hili ndilo lililowawezesha kuwahamisha watu kutoka mafichoni katika jiji la Beijing na kuwavusha mpaka.

Uingereza na Marekani zilihusika tu pale watu hao walipofika Hong Kong na wapolihitaji kujua wanaende wapi.

Yan anakumbuka kutembelewa na “bwana wa Kingereza” ambaye hakuwahi kutaja jina lake, na alimsaidia Yan kuanadaa makaratasi.

“Ni afadhali uende Marekani, si Uingereza,” mtu huyo alimwambia Yan. Baada ya siku chache, Yan alikuwa Los Angeles. Chaohua Wang pia aliishia Marekani.

Kwanini isiwe England?

K

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, 1996: Chris Patten (kushoto) alikuwa gavana wa mwisho wa kikoloni wa Hong Kong

Maafisa wa zamani wameiambia BBC, Uingereza ilisita kuwapokea waandamanaji wa Tiananmen kwa sababu ilikuwa ikitaka kuepuka kuikasirisha China wakati wa maandalizi ya kuiachia Hong Kong mwaka 1997.

Mkataba ulikuwa umetiwa saini na Uingereza mwaka 1984, lakini matukio ya Tiananmen Square miaka mitano baadaye yalizua maswali magumu kuhusu mustakabali wa Hong Kong.

Mnamo 1992, Waziri wa zamani wa baraza la mawaziri la Conservative Chris Patten alikua gavana wa mwisho wa Hong Kong.

Anasema alidhamiria kusimika demokrasia, kwa matumaini kwamba ingedumu baada ya makabidhiano, na alitangaza mapendekezo ya mageuzi ya kidemokrasia ya taasisi za Hong Kong, yenye lengo la kupanua wigo wa kupiga kura katika uchaguzi.

Kulikuwa na upinzani dhidi ya mageuzi hayo sio tu kutoka kwa uongozi wa China lakini pia kutoka kwa wale wa London ambao hawakutaka kuiudhi Beijing.

"Jukumu langu kuu lilikuwa kujaribu kuwapa watu wa Hong Kong nafasi nzuri zaidi ya kuendelea kuishi kwa uhuru na ustawi, na hali iwe hivyo hata baada ya 1997," anasema Lord Patten.

Anasema alikuwa anajua kuhusu operesheni ya Yellow Bird - lakini hakuhusika.

Yellow Bird iliisha usiku wa mvua mwezi Julai 1997 wakati Hong Kong ilipokuwa eneo huru chini ya China. Baada ya miaka michache, uhuru ambao Patten alikuwa akijaribu kuuweka, ulikuwepo. Lakini katika muongo mmoja uliopita, China - chini ya Xi Jinping - imechukua hatua za kimabavu zaidi na imejaribu kuileta Hong Kong chini ya utiifu wake.

Kuwindwa na China

K

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, 1997: Prince Charles na rais wa China Jiang Zemin katika makabidhiano ya Hong Kong

Yan alichukua uraia wa Marekani na kuishi Marekani. Alijiunga na jeshi la Marekani na akahudumu nchini Iraq kama kasisi wa kijeshi.

Huenda alifikiri kwamba mkono wa Chama cha Kikomunisti cha China haungeweza kumfikia katika nyumba yake mpya, lakini alikosea.

Mwaka 2021, aliamua kugombea ofisi ya umma. Alisimama kama mgombea katika mchujo wa chama cha Democratic katika jimbo moja la New York.

Alianza kugundua matukio yasiyo ya kawaida wakati wa kampeni yake. Magari ya ajabu yalimfuata na katika hafla za kampeni, kuna watu walikuwa wakijaribu kumzuia asizungumze.

Alielewa kwa nini hayo yanatokea pale FBI walipokuja kuzungumza naye. Mpelelezi binafsi wa Marekani aliwaambia FBI kuwa alifuatwa na mtu mmoja nchini China, ambaye alimwomba afanye uchunguzi kuhusu Yan. Inaonekana kuwa wazo la muandamanaji wa zamani wa Tiananmen kuingia katika Bunge la Marekani halikubaliki China.

"Alimwambia mpelelezi huyo kwamba walihitaji kudhoofisha ugombeaji wake," anasema wakala wa FBI Jason Moritz.

FBI waliweza kufuatilia matukio huku Mchina huyo akipendekeza kwa mpelelezi kufichua mambo mabaya ya Yan. Ikiwa hakuweza kupata chochote, aliagizwa kutengeneza matukio. Ikiwa hilo halikufaulu, hata kumpiga au kuandaa ajali ya gari.

"Wanataka kuzima na kuua kampeni yangu," Yan anaelezea.

Mtu aliyekuwa akimwagiza mpelelezi wa kibinafsi, FBI ilielewa kuwa alikuwa akifanya kazi kwa niaba ya Wizara ya Usalama ya Nchi ya China. Alifunguliwa mashtaka lakini hawakuweza kumkamata kwa sababu alikuwa nje ya Marekani.

China imekanusha mara kwa mara madai ya kuingilia siasa za Marekani. Lakini hii si kisa pekee ambapo inadaiwa kuwa inawasaka wale inaowachukulia kuwa ni wapinzani katika nchi nyingine. Kumekuwa na madai ya watu kufuatiliwa nchini Uingereza na Marekani na watu binafsi kushinikizwa kurudi China au kunyamaza.

Hadithi ya Yan inafichua kwamba China inayozidi kujiamini na kujenga udhibiti nyumbani, pia imejaribu kupanua ufikiaji wake nje ya nchi. Na hilo linazidi kusababisha msuguano katika masuala ya ujasusi, ufuatiliaji na haki za binadamu.

Wakati huo huo, ujumbe wa Yan kwa serikali za Magharibi wakati wa kushughulika na China ni: "Lazima wawe waangalifu."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi