Got a TV Licence?

You need one to watch live TV on any channel or device, and BBC programmes on iPlayer. It’s the law.

Find out more
I don’t have a TV Licence.

Habari za moja kwa moja

Na Asha Juma

time_stated_uk

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja,

  2. Chad yawapeleka wanajeshi katika mji mkuu baada ya matokeo ya uchaguzi

    XX

    Idadi kubwa ya wanajeshi na maafisa wa polisi wanashika doria kwenye mitaa ya mji mkuu wa Chad, N'Djamena, baada ya kiongozi wa kijeshi Mahamat Déby kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais.

    Hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa Alhamisi usiku, walinzi wa rais walikuwa wameegesha magari mengi ya kivita kwenye makutano ya njia kuu, shirika la habari la AFP linaripoti.

    Succes Masra, mgombea wa upinzani ambaye pia ni waziri mkuu wa Bw Déby, alitangaza Alhamisi usiku kwamba ameshinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi.

    Bw Masra alisema ushindi umenyakuliwa "kutoka kwa watu" na kutoa wito kwa wafuasi wake "kupinga hilo ... kwa utulivu".

    Jenerali Déby, 40, alitawazwa kama kiongozi wa Chad na jeshi baada ya baba yake, Idriss Déby Itno, kuuawa wakati wa vita na vikosi vya waasi mnamo Aprili 2021.

    Ushindi wake unamaanisha kwamba utawala wa miaka 34 wa familia ya Déby utaendelea.

    Kumekuwa na ripoti ya upigaji kura kukumbwa na dosari.

    Wanasiasa10 ambao walikuwa na matumaini ya kugombea wazuiliwa na baraza la katiba kwa sababu ya "kasoro", ambayo wengine wanasema ilichochewa kisiasa.

  3. Ureno ina 'wasiwasi' kuhusu ushirikiano kati ya Urusi na Sao Tome

    Serikali ya Ureno imesema "ina wasiwasi mkubwa" baada ya Sao Tome na Principe - koloni lake la zamani - hivi karibuni kutia saini makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na Urusi.

    Waziri wa mambo ya nje Paulo Rangel amesema Ureno na mataifa mengine ya Ulaya yameshangazwa, yana wasiwasi na hatua hiyo.

    Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Ureno, aliikosoa Urusi kwa kile alichokiita vita vyake vya uvamizi nchini Ukraine.

    Makubaliano ya hivi majuzi kati ya Moscow na Sao Tome yanaruhusu Urusi kutuma ndege na meli za kivita kwenye visiwa vya Sao Tome

    Nchi nyingine kadhaa za Kiafrika katika kanda hiyo zimekuwa zikiimarisha uhusiano na Urusi na katika visa vingine kusitisha makubaliano na Ufaransa na Marekani.

  4. Tiwa Savage: Siku zote nilitaka kuwa muigizaji

    Tiwa Savage

    Mwimbaji wa Nigeria Tiwa Savage anajulikana kama "Queen of Afrobeats" lakini sasa anakishusha kipaza sauti kwa muda ili kuigiza kwa mara ya kwanza katika filamu mpya, Water & Garri.

    Filamu inayooneshwa sasa kwenye Amazon Prime inamuonesha mwanadada anayeitwa Aisha, aliyeigizwa na Tiwa Savage, mbunifu mahiri wa mitindo ambaye anarejea nyumbani Nigeria baada ya miaka 10 nchini Marekani.

    Ingawa mwimbaji huyo aliyeteuliwa na Grammy amewavutia watu kwa sauti yake nyororo, aliiambia podikasti ya BBC Focus on Africa kwamba uigizaji siku zote ni njia anayotaka kuifuata.

    "Ninaheshimu sana waigizaji sasa. Ni saa nyingi na unakuwa mtu mwingine kwa muda mrefu," alisema. Aliiambia BBC haikuwa "rahisi".

    Ingawa filamu inaweza kuwa mpya, msukumo unatoka kwa EP yake ya mwaka 2021 ya jina moja. Filamu hiyo hapo awali ilikusudiwa kuwa video inayoambatana na mradi huo, lakini alisema walipoanza kurekodi "ilikuwa nzuri sana" waliamua kuifanya kuwa filamu ndefu.

    Nyimbo za filamu zinaangazia nyota wengine wa Nigeria kama vile Olamide na mwimbaji aliyeteuliwa na Grammy Ayra Starr.

    "Kuna hisia za furaha unapofikiria maji na garri. Tulikuwa tunakula hivyo sana tulipokuwa tukikua," alisema.

    Aliongeza kuwa garri, ambayo muhogo wa kusindika, na maji ni michanganyiko isiyo ya kawaida, lakini yanapochanganywa pamoja hutoa kitu kizuri.

  5. Ukraine yasema imezima shambulio la Urusi kaskazini mashariki mwa Kharkiv

    Mapigano makali yanaendelea, na raia wanahamishwa kutoka wilaya ya Vovchansk

    Ukraine imesema kuwa imezima shambulio la kivita la Urusi katika eneo la kaskazini-mashariki la Kharkiv, baada ya vikosi vya Moscow kushambulia mpaka na kutaka kuvunja njia za kujihami.

    Mkuu wa mkoa wa Kharkiv Oleh Syniehubov alisema vikundi vya upelelezi vya Urusi vilijaribu kupenya mpaka, na kuongeza kuwa "hakuna hata mita moja iliyopotea". "Ukraine ilikutana nao huko na askari: brigedi na mizinga," Rais Volodymyr Zelensky aliuambia mkutano wa waandishi wa habari.

    Makamanda wa Ukraine wamekuwa wakitarajia mashambulizi ya majira ya joto kwa muda, pengine hata jitihada za kuuteka mji mkuu wa kikanda wa Kharkiv.

    Lakini maafisa wanasisitiza Urusi haina rasilimali za kufanya hivyo.

    Wizara ya ulinzi mjini Kyiv ilisema shambulio hilo lilianza na mashambulizi makubwa ya mabomu katika makazi madogo.

    Mashambulizi ya anga ya Urusi yalishambulia Vovchansk "kwa kutumia mabomu ya angani ya kuongozwa" kwa msaada wa mizinga, kabla ya "vikundi vidogo vya skauti" vya Kirusi kuingia.

    Mkuu wa eneo la Vovchansk alisema kuwa mji huo ulishambuliwa vikali kuanzia asubuhi ya Ijumaa na raia walikuwa wakihamishwa.

    Mtu mmoja aliuawa na wengine watano kujeruhiwa katika shambulio hilo, Bw Syniehubov alisema. "TakribanI saa 05:00, kulikuwa na jaribio la adui kuvunja safu yetu ya ulinzi chini ya kifuniko cha magari ya kivita. Kufikia sasa, mashambulizi haya yamerudishwa nyuma, mapigano ya nguvu tofauti yanaendelea," wizara ya ulinzi ilisema.

    Mapigano makali yanaendelea, na raia wanahamishwa kutoka wilaya ya Vovchansk huku wanajeshi wa akiba wakiingia, maafisa waliongeza.

    Unaweza kusoma:

    Kwanini kuna wasiwasi kwamba Urusi inatumia makombora ya Korea Kaskazini nchini Ukraine?

    Sababu tatu zinazomfanya Putin kuwa na nguvu zaidi ya awali

  6. Zanu-PF haiingilii uchaguzi wetu, ANC yasisitiza

    Afrika Kusini inatazamiwa kufanya uchaguzi mkuu tarehe 29 Mei
    Image caption: Afrika Kusini inatazamiwa kufanya uchaguzi mkuu tarehe 29 Mei

    Chama tawala nchini Afrika Kusini, ANC, kimetetea kualika chama tawala cha Zimbabwe nchini humo kabla ya uchaguzi.

    Chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini kililaani mwaliko huo kama jaribio la "kuchafua" mchakato wa uchaguzi.

    Chama cha Democratic Alliance (DA) kilisema ombi la Zanu-PF kuwa "sehemu ya programu ya kampeni ya uchaguzi [ya ANC] ni sawa na kuingiliwa kwa kisiasa na uchaguzi wetu".

    DA ilisema Zanu-PF haikustahili kuwa mwangalizi katika uchaguzi huo, na kuongeza kuwa itawasilisha malalamishi yake kwa tume ya uchaguzi.

    Kujibu suala hilo, Naibu Katibu Mkuu wa ANC Nomvula Mokonyane alishutumu upinzani kwa "mkanganyiko kati ya shughuli za chama na hadhi ya waangalizi kulingana na michakato ya [tume ya uchaguzi]".

    Bi Mokonyane alisema ANC ilialika Zanu-PF nchini kama mgeni. Chama chake "kina utamaduni wa muda mrefu wa kualika vyama vya ukombozi kutoka katika bara zima la Afrika na kwingineko kama wageni", aliongeza.

    Mapema wiki, gazeti linalodhibitiwa na serikali ya Zimbabwe lilimnukuu Katibu Mkuu wa Zanu-PF Obert Mpofu akisema chama hicho kimealikwa na ANC "kuwa sehemu ya mchakato wao wa uhamasishaji katika siku chache zilizopita za kampeni".

    Maelezo zaidi:

    Je, chama cha ANC kitaathiriwa na kujiondoa kwa Jacob Zuma?

    Julius Malema: Mwanasiasa anayeiongoza EFF katika uchaguzi wa 2024 wa Afrika Kusini

    Waafrika Kusini wanavyohisi kuhusu miaka 30 ya uhuru

  7. Wakenya wapanda miti kuwakumbuka waliofariki katika wa mafuriko

    xx

    Maafisa wa Kenya wanaongoza zoezi la upandaji miti kote nchini kama sehemu ya siku ya kitaifa ya maombolezo ya waliofariki katika mafuriko yaliyosababisha vifo vya hivi majuzi.

    Rais William Ruto ametoa wito kwa wakenya kujumuika kupanda miti akisema mafuriko na ukame ni masuala ya mazingira.

    Akizungumza katika hafla ya upandaji miti katikati mwa Kenya siku ya Ijumaa, alimtaka kila Mkenya kupanda angalau miti 50 ili kutimiza lengo la siku hiyo la kupanda miti milioni 200.

    Maafisa wengine wa serikali, wakiwemo mawaziri, wanaongoza zoezi sawa na hilo kote nchini.

    Mafuriko katika wiki za hivi majuzi yamesababisha vifo vya takriban watu 230 na kuwafanya zaidi ya robo milioni kuyahama makazi yao.

    Serikali ilitangaza Ijumaa kuwa sikukuu ya umma kwa Wakenya kupanda miti na kuwakumbuka waliofariki katika mkasa huo.

  8. Harry na Meghan waanza ziara ya siku tatu nchini Nigeria

    xx

    Mwanamfalme Harry na mke wake Meghan wamewasili nchini Nigeria kwa ziara ya siku tatu.

    Hii ni safari yao ya kwanza nchini humo kama wanandoa, na inakuja baada ya Mwanamfalme Harry kuhitimisha ziara fupi ya London, ambapo aliiambia BBC ilikuwa "ni vyema" kurejea Uingereza.

    Prince Harry na Meghan walialikwa na mkuu wa ulinzi wa Nigeria, Jenerali Christopher Musa, na watakutana na wafanyikazi waliojeruhiwa.

    Ziara yao ni sehemu ya mfululizo wa matukio yanayohusishwa na Michezo ya Invictus, tukio la michezo kwa wanaume na wanawake wa kijeshi waliojeruhiwa iliyoanzishwa na Prince Harry ambayo inaadhimisha mwaka wake wa 10 mwaka huu.

    Wanandoa hao waliwasili mjini Abuja leo (Ijumaa) asubuhi, na kuanza ziara yao kwa kutembelea Lightway Academy, shule ya msingi na sekondari katika mji mkuu.

    Walipokelewa na wacheza ngoma za asili na kukutana na baadhi ya watoto wa shule ya msingi.

    Kundi moja la wanafunzi wa mwaka wa tano waliiambia BBC kwamba walifurahi sana kuwa na duke na duchess kutembelea, wakisema wanatumai itainua hadhi ya shule yao.

    Wanandoa hao kisha waliendelea na uzinduzi wa mkutano wa kilele wa afya ya akili wa siku mbili, baada ya hapo mkuu huyo ataelekea katika kituo cha ukarabati wa kijeshi huko Kaduna.

    XX
    XX
    XX
  9. Rais wa zamani wa Zambia aonywa kujiepusha na shughuli 'zinazovutia mikusanyio ya watu'

    Edgar Lungu
    Image caption: Rais wa zamani wa Zambia Edgar Lungu

    Polisi nchini Zambia wameonya kuwa Rais wa zamani Edgar Lungu anakabiliwa na tishio la kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa "kujihusisha na shughuli zinazovuruga utulivu na usalama wa umma".

    Hii ni baada ya umati wa watu kumiminika Bw Lungu alipokuwa akizunguka mji mkuu, Lusaka, Alhamisi kutathmini gharama ya juu iliyoripotiwa ya kufanya biashara jijini.

    Bw Lungu alisema "anashangazwa na jinsi bei za bidhaa zimepanda" chini ya serikali ya Rais Hakainde Hichilema.

    Umati wa watu ulionekana wakimpungia mkono kiongozi huyo wa zamani alipokuwa akipita katika mitaa ya jiji hilo.

    Katika taarifa polisi walisema kuwa Bw Lungu alisababisha "msongamano mkubwa wa magari" wakati wa ziara yake.

    "Tunataka kusisitiza kwamba vitendo kama hivyo vinaunda mkusanyiko usio halali na bila kujali hadhi ya mtu ya zamani kama mkuu wa nchi, uzingatiaji wa sheria hauwezi kujadiliwa," msemaji wa polisi, Rae Hamoonga, alisema.

    Alimtaka rais huyo wa zamani kuendesha shughuli zake "ndani ya mipaka ya sheria na kujiepusha na vitendo vinavyovuruga amani na utulivu wa umma".

    "Kushindwa kuzingatia kutasababisha hatua muhimu za kisheria kuchukuliwa." Kiongozi huyo wa zamani alionywa mwaka jana dhidi ya kukimbia hadharani, kwani polisi walielezea mazoezi yake ya kila wiki kama "harakati za kisiasa".

    Bw Lungu, ambaye alipoteza urais kwa Rais Hichilema mwaka wa 2021, ametangaza kurejea kwenye siasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2026.

  10. Mazungumzo ya amani ya Sudan Kusini yaanza jijini Nairobi

    Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
    Image caption: Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir anatumai mazungumzo hayo yataleta matokeo chanya

    Mazungumzo ya amani yanayohusisha serikali ya Sudan Kusini na wawakilishi wa upinzani yalianza katika mji mkuu wa Kenya Nairobi siku ya Alhamisi.

    Mazungumzo hayo ni kati ya serikali na makundi ya waasi ya upinzani ambayo hayakuwa sehemu ya makubaliano ya mwaka 2018 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano.

    Baadhi ya masuala katika mkataba wa 2018, ni pamoja na kuunganisha kikosi cha usalama, yamesalia kuwa bora.

    Upinzani ulikuwa umeitisha duru mpya ya mazungumzo kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Disemba, kama sehemu ya hatua ya kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa uwazi.

    Marais kadhaa wa Afrika wanaohudhuria mazungumzo hayo ya kutaka kuhitimishwa kwa mzozo nchini Sudan Kusini umedumaza uchumi wa nchi hiyo kwa miaka kadhaa.

    Miongoni mwao ni marais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Lazarus Chakwera wa Malawi, Hakainde Hichilema wa Zambia, Nangolo Mbumba wa Namibia na Faustin-Archange Touadera wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

    Mwenyeji, Rais wa Kenya William Ruto, alisema ana nia ya upatanishi wa pamoja na wa nyumbani ili kumaliza mzozo huo.

    "Mpango huu ni mfano wa sera ya Afrika ya Afrika ya kutatua changamoto za Afrika, inayochangia mpango wa 'Kunyamazisha Bunduki Afrika' na kukuza mazingira ya kuleta mabadiliko nchini Sudan Kusini, ukanda wetu na bara zima la Afrika," alisema.

    Rais wa Sudan Kusini alisema anatumai upatanishi huo utakuwa na matokeo chanya kabla ya uchaguzi mkuu.

    "Tunatumai kwamba vikundi vya upinzani vina imani sawa na hamu ya amani nchini Sudan Kusini, ambayo, ikipatikana kikamilifu, italeta utulivu wa milele na maendeleo ya kiuchumi kikanda," alisema.

  11. Afrika Kusini: Mahakama ya juu kusikiliza rufaa dhidi ya ugombea urais wa Zuma

    Zuma

    Mahakama ya juu nchini Afrika Kusini inajiandaa kusikiliza rufaa kuhusu iwapo rais wa zamani Jacob Zuma atastahili kugombea katika uchaguzi mkuu ujao.

    Bw Zuma, 82, anaongoza chama kipya cha upinzani, Umkhonto we Sizwe (MK) chama, ambacho wachambuzi wanasema kinaweza kuvuruga matokeo ya uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Mei.

    Mnamo Aprili Mahakama ilisema kwamba alikuwa huru kugombea baada ya tume ya uchaguzi kumzuia kwa kupuuza hukumu ya mahakama.

    Ilikuwa imedai kuwa katiba inawazuia watu kushikilia ofisi ya umma ikiwa watapatikana na hatia ya uhalifu na kuhukumiwa kifungo cha zaidi ya maka mmoja jela.

    Bw Zuma alihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela mwaka wa 2021 kwa kukosa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa ufisadi, na alitumikia kifungo hicho kwa miezi mitatu kabla ya kuachiwa kwa misingi ya kiafya.

    Soma pia:

    Je, chama cha ANC kitaathiriwa na kujiondoa kwa Jacob Zuma?

  12. Watengeneza maudhui yaTiktok washtakiwa kwa kufanya maigizo ya wizi katika kituo cha polisi Kenya

    .

    Watengeneza maudhui wanne wa TikTok waliokamatwa kwa kurekodi video ya maigizo ya wizi uliofanywa nje ya kituo cha polisi katika pwani ya Kenya wameshtakiwa kwa kuchapisha habari za uongo, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

    Watengenezaji maudhui hao akiwemo mvulana wa umri wa miaka 17, walikamatwa Jumatano katika kaunti ya Kilifi baada ya video hiyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

    Katika video hiyo ya kuigiza, mwanamume mmoja anatoka katika kituo cha polisi cha Kilifi na kunyang'anywa begi lake na watu wengine wawili waliokuwa kwenye pikipiki inayomsubiri, almaarufu boda boda.

    Polisi walisema watu hao walikamatwa baadaye baada ya kutambuliwa kupitia kamera ya CCTV katika kituo hicho.

    Washukiwa hao walichapisha video hiyo kwenye mtandao wa TikTok ikiwa na nukuu "majambazi nje ya kituo cha polisi cha Kilifi", ambayo walijua ni ya uwongo, mahakama ilisikiza kesi hiyo Alhamisi.

    Wanne hao walikanusha mashtaka na walipewa dhamana ya $1,500 (£1,200), tovuti ya habari ya Nation iliripoti.

    Kesi hiyo itasikizwa tarehe 30 Julai.

  13. Operesheni ya Israel yaziacha hospitali za Rafah zikiwa na wagonjwa kipita kiasi

    .

    Hata bila uvamizi wa ardhini wa Israel, vituo vya matibabu vya Rafah vimekuwa na wagonjwa wengi kupita kiasi.

    Madaktari wanasema zaidi ya watu milioni moja wanaojihifadhi katika mji wa kusini wa Gaza wako katika hatari ya kukosa huduma za afya baada ya jeshi la Israel kuanza operesheni "ndogo" dhidi ya Hamas kwenye viunga vyake vya mashariki siku ya Jumatatu.

    Hospitali kubwa kati ya tatu za jiji hilo ambayo kwa kiasi kikubwa ni sehemu kidogo inayofanya kazi, Abu Youssef al-Najjar, ilibidi watu kuondoka kwa haraka siku iliyofuata baada ya wafanyikazi kupokea amri ya kuhamishwa na kuarifiwa kulikuwa na mapigano eneo la karibu.

    Kitengo cha kusafisha damu katika hospitali hiyo ndio pekee kilichosalia huko Gaza kama mwokozi kwa wagonjwa wanaougua figo kwa kushindwa kufanya kazi.

    Israel pia imezuia ufikiaji wa Hospitali ya karibu ya Gaza ya Khan Younis, ambapo wagonjwa mahututi walikuwa wakipewa rufaa ya upasuaji.

    Wakati huo huo, hospitali ya kuu ya uzazi ya Imarati huko Rafah imekuwa na shughuli nyingi za wanawake kujifungua watoto kila siku, na inajitahidi kukabiliana na ongezeko la kesi za dharura licha ya ukosefu wa uwezo, wafanyakazi na vifaa.

    Daktari mmoja katika hospitali hiyo, ambayo kabla ya vita ilikuwa na vitanda vinne pekee vya wagonjwa mahututi, alisema hali hiyo ni "janga".

  14. Mabaki ya panya yapatikana kwenye mkate Japani

    .

    Kampuni moja inayotengeneza mkate maarufu nchini Japani imetoa agizo la kurejeshwa kwa mikate elfu kadhaa na wateja kurejeshewa pesa zao baada ya mabaki ya panya kupatikana kwenye bidhaa hiyo.

    Takriban pakiti 104,000 za mkate mweupe uliokatwa vipande vipande wa Shirika la Pasco Shikishima umeondolewa kwenye rafu. Sehemu za panya mweusi ziligunduliwa katika takriban mikate miwili.

    Mkate wa Pasco ni chakula kikuu katika kaya nyingi za Kijapani na unapatikana kila mahali katika maduka makubwa na maduka madogo kote nchini humo.

    Hakujakuwa na ripoti hadi sasa za mtu yeyote kuugua kama matokeo ya tukio hilo, Pasco ilisema katika taarifa mapema wiki hii.

    "Tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa wateja wetu, washirika wa kibiashara na pande zote zinazohusika," ilisema.

    Mkate huo ulitengenezwa katika kiwanda kimoja huko Tokyo, ambacho shughuli zake zimesitishwa kwa sasa.

    Pasco haikueleza ni namna gani mabaki ya panya yalivyoishia kwenye bidhaa zake, lakini iliahidi "kufanya tuwezavyo kuimarisha udhibiti wetu wa ubora ili hili lisijirudie tena".

    Kampuni hiyo imechapisha fomu kwenye tovuti yake kwa wateja walioathirika kutuma maombi ya kurejeshewa pesa zao mtandaoni.

    Bidhaa zake pia zinasafirishwa kwenda Marekani, Uchina, Australia, na Singapore, kati ya nchi zingine.

    Agizo la kurejeshwa kwa chakula ni nadra sana nchini Japani, nchi yenye viwango vya juu vya usafi wa mazingira.

  15. Mwanajeshi wa jeshi la Wanahewa Marekani apigwa risasi na kuuawa na polisi

    .

    Polisi huko Florida nchini Marekani wametoa hadharani picha za kamera kutoka kwa naibu aliyempiga risasi mwanajeshi wa Jeshi la Wanahewa la Marekani nyumbani kwake.

    Afisa mwandamizi katika jeshi la wanahewa Roger Fortson, ambaye alikuwa na umri wa miaka 23, alipelekwa hospitali ambapo alifariki, maafisa walisema.

    Wakili wa familia ya mwathiriwa, akimnukuu shahidi, alidai polisi walivamia nyumba tofauti na waliokuwa wanapaswa kwenda.

    Hata hivyo, polisi wamepinga madai hayo na kusema naibu huyo alijibu kwa kujilinda baada ya kumuona Fortson akiwa amejihami kwa bunduki.

    Mwanahewa huyo alipigwa risasi tarehe 3 Mei nyumbani kwake, iliyoko umbali wa maili 5 (8km) kutoka Mrengo wa Operesheni Maalum huko Hurlburt Field, Florida, anakoishi.

    Naibu aliyempiga risasi - ambaye polisi hawajamtaja - tangu wakati huo amepewa likizo.

    Afisa wa Kaunti ya Okaloosa Eric Aden alisema ufyatuaji risasi huo unachunguzwa na Idara ya Utekelezaji Sheria ya Florida na Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali.

    Bw Aden aliahidi uwepo wa "uwazi na uwajibikaji" lakini akaongeza: "Uchunguzi huu unachukua muda."

    "Lakini nataka kukuhakikishia kwamba hatujifichi, au hatuchukui hatua yoyote ambayo ingesababisha uamuzi wa haraka wa Bw Fortson au naibu wetu."

    Afisa huyo alionyesha video ya dakika nne iliyochukuliwa kutoka kwa kamera iliyokuwa imevaliwa mwilini na naibu ambaye alifyatua risasi.

  16. Iran yawaachilia huru raia watano wa India kutoka kwa meli walioikamata mwezi uliopita

    .

    Iran imewaachia huru raia watano wa India kutoka kwa meli MSC Aries walioikamata.

    Raia hao watano wa India watafukuzwa kutoka Iran na kurejeshwa nchini India jioni hii.

    Ubalozi wa India nchini Iran ulitoa taarifa hii kwenye mtandao wa kijamii wa X

    Jeshi la Wanamaji la Iran lilikuwa limekamata meli ya mizigo ya MSC Aries iliyokuwa ikienda India tarehe 13 Aprili.

    Kuna wafanyakazi 25 kwenye meli. Kati ya hao, 17 ni raia wa India.

    Iran ilichukua hatua hii huku kukiwa na mvutano unaoendelea na Israel. Mmiliki wa meli hii ni mfanyabiashara wa Israel.

    Wafanyakazi wa meli hiyo pia walijumuisha mwanamke pekee, Ann Tessa Joseph. Aliachiliwa siku chache baada ya meli hiyo kukamatwa.

  17. Bosi wa Ligi ya Premia aliyeshinda ombi la kutotajwa jina mahakamani ahusishwa na kesi ya unyanyasaji wa ngono

    .

    Bosi wa Ligi Kuu ya Uingereza ameshinda agizo la Mahakama Kuu la kutotajwa jina katika kesi dhidi yake ya madai ya kumdhulumu kingono msichana wa miaka 15.

    Anashtakiwa kwa uharibifu uliokithiri na mwanamke ambaye anasema makosa hayo yalifanyika miongo miwili iliyopita.

    Uchunguzi wa BBC tayari umefichua kuwa bosi huyo bado anashikilia nafasi hiyo licha ya uchunguzi wa polisi kuhusu madai ya ubakaji wa msichana tofauti, 15 .

    Kesi dhidi ya bosi huyo iliwasilishwa mwezi Januari, na mawakili wake wamefanikiwa kutetea mahakamani kwamba amri itekelezwe kuzuia jina lake kutotolewa na vyombo vya habari.

    Mwalimu Stevens, ambaye ni kama jaji katika Kitengo cha Kifalme cha Mahakama Kuu, alisema katika nyaraka za mahakama kwamba, alizingatia haki za binadamu kwa maisha ya kibinafsi na ya familia, pamoja na uhuru wa kujieleza, wakati wa kufanya uamuzi wake.

    Alihitimisha mwezi uliopita kwamba ulinzi wa utambulisho wa bosi huyo ulikuwa muhimu ili "kuwezesha kupatikana kwa haki", akiongeza kuwa "hakuna nadhari kutoka kwa umma inayopinga" jina lake kufichwa.

    Sheria za faragha nchini Uingereza zinatumika kuwatambua washukiwa katika hatua za awali za uchunguzi wa polisi, hata hivyo vyombo vya habari kwa kawaida vinaruhusiwa kuripoti kesi mahakamani, zikiwemo mahakama za kiraia.

    Mapema mwaka huu, BBC iliiomba mahakama nyaraka kuhusiana na kesi hii lakini mahakama haikumjibu mwanahabari huyo aliyetoa ombi hilo au kuwapa agizo la ombi la kutotajwa jina, kwa hiyo BBC haikuweza kutoa maelezo ya kupinga amri hiyo kabla uamuzi wa hakimu.

  18. Kiongozi wa kijeshi wa Chad ashinda uchaguzi wa urais

    TH

    Mtawala wa kijeshi wa Chad Mahamat Déby ametangazwa mshindi rasmi wa uchaguzi wa urais, na hivyo kuhalalisha kushikilia kwake madaraka.

    Jenerali Déby alishinda 61.3% ya kura, kwa mujibu wa baraza la uchaguzi la taifahilo, likitoa matokeo ya muda, huku mpinzani wake wa karibu, Waziri Mkuu Succes Masra, akipata18.53%.

    Bw Masra alikuwa ametangaza mapema kwamba amepata "ushindi mkubwa" katika duru ya kwanza ya upigaji kura, na kwamba ushindi uliibiwa "kutoka kwa watu".

    Jenerali Déby, 40, alitawazwa kama kiongozi wa Chad na jeshi baada ya baba yake, Idriss Déby Itno, kuuawa wakati wa vita na vikosi vya waasi mnamo Aprili 2021.

    Ushindi wake unamaanisha kwamba utawala wa miaka 34 wa familia ya Déby utaendelea.

    Matokeo ya uchaguzi wa Jumatatu yalitangazwa wiki mbili mapema kuliko ilivyotarajiwa.

    Yanastahili kuthibitishwa na baraza la katiba.

    Kabla tu ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa, Waziri Mkuu Masra alidai kushinda katika matangazo ya moja kwa moja kwenye Facebook, na kutoa wito kwa wafuasi wake na vikosi vya usalama kupinga kile alichosema ni jaribio la Jenerali Déby "kuiba ushindi kutoka kwa watu".

    "Idadi ndogo ya watu binafsi wanaamini wanaweza kuwafanya watu kuamini kuwa uchaguzi ulishindwa kwa mfumo ule ule ambao umekuwa ukitawala Chad kwa miongo kadhaa," alisema.

    Chad inakuwa nchi ya kwanza kati ya nchi ambazo jeshi lilinyakua mamlaka katika Afrika Magharibi na Kati katika miaka ya hivi karibuni kufanya uchaguzi na kurejesha utawala wa kiraia.

    Lakini wakosoaji wanasema kwa kuchaguliwa kwa Jenerali Déby, machache yamebadilika.

    Upigaji kura wa Jumatatu kwa kiasi kikubwaulikuwa wa amani lakini takriban mpiga kura mmoja aliuawa, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

    Pia kumekuwa na ripoti za upinzani kuhusu dosari siku ya kupiga kura.

    Wanasiasa kumi ambao walikuwa na matumaini ya kugombea walitengwa na baraza la katiba kwa sababu ya "kasoro", ambayo wengine wanasema ilichochewa kisiasa.

    Mpinzani mwingine aliyyetarajiwa kuwania urais, na binamu wa Jenerali Déby, Yaya Dillo, aliuawa na vikosi vya usalama mwezi Februari wakati akidaiwa kuongoza mashambulizi dhidi ya Shirika la Usalama la Taifa katika mji mkuu, N'Djamena.

  19. Urusi inaishambulia Ukraine kwa makombora kutoka pande mbili kwa wakati mmoja

    .

    Urusi inaifyatulia Ukraine makombora ya ballistic kutoka kusini na kaskazini kwa wakati moja.Kikosi cha anga cha Ukraine Air Force kilitangaza tishio la makombora ya ballistic kutoka Crimea, na mifumo ya uangalizi iliripoti shambulizi hilo.

    Pia kulitolewa onyo la uvamizi wa anga katika majimbo ya kusini, ingawa hali imerejea kuwa ya kawaida baada ya shambulizi lililotekelezwa na watu wa kujitolea muhanga.

    Bado mashambulizi yanaendelea upande wa kaskazini.

    Mifumo ya taarifa na ufuatiliaji wa vita iliripoti kurushwa kwa makombora manne mfululizo na kutokea kwa mlipuko eneo la Kharkov.

    Meya wa jiji, Ogor Terekhov, aliandika kwenye telegram kwamba shambulio hilo lilitokea eneo la makazi ya watu na kwamba majengo ya kibinafsi ya makazi yaliteketea kwa moto uliosababishwa ni mashambulizi hayo.

    "Tutaelezea taarifa kamili kuhusu waathiriwa", meya aliongeza.

    Soma zaidi:

    Yafahamu makombora ya masafa marefu ambayo Marekani imeipa Ukraine

  20. Netanyahu asema Israel inaweza 'kujitegemea' ikiwa Marekani itasita kuipa silaha

    .

    Benjamin Netanyahu amesema Israel inaweza "kujitegemea" baada ya Marekani kuonya kuwa inaweza kusitisha usambazaji wa silaha ikiwa waziri mkuu wa Israel ataamuru uvamizi kamili wa Rafah huko Gaza.

    "Tukihitaji ... tutajitegemea. Nimesema ikibidi tutapigana kwa jino na ukucha," alisema.

    Rais wa Marekani Joe Biden alisema atazuia baadhi ya silaha ikiwa ni pamoja na mizinga ikiwa Rafah itavamiwa.

    Marekani tayari imesitisha shehena ya mabomu kutokana na hofu ya vifo vya raia.

    Bw Netanyahu siku ya Alhamisi hata hivyo alikariri vita vya mwaka 1948 vya kutupilia mbali maonyo kutoka Marekani, mshirika wa karibu wa Israel.

    "Katika Vita vya Uhuru miaka 76 iliyopita, tulikuwa wachache dhidi ya wengi," alisema "Hatukuwa na silaha. Kulikuwa na vikwazo vya silaha kwa Israel, lakini kwa nguvu kubwa ya kiroho, ushujaa na umoja kati yetu – sisi tulikuwa washindi."

    Alisema kuwa Israel ina "zaidi ya kucha zetu" ikiwa Bw Biden atasitisha usambazaji wa silaha. "Na kwa nguvu hiyo ya kiroho, kwa msaada wa Mungu, pamoja tutakuwa washindi."

    Yoav Gallant, waziri wa ulinzi wa Bw Netanyahu, wakati huo huo alisema "maadui wa Israel pamoja na ... marafiki bora" wanapaswa kuelewa kwamba nchi yake "haiwezi kutawaliwa. Tutasimama imara, tutafikia malengo yetu."

    Maoni hayo yanawadia saa chache baada ya Umoja wa Mataifa kusema zaidi ya watu 80,000 wametoroka Rafah tangu Jumatatu huku kukiwa na mashambulizi ya mara kwa mara na vifaru vya Israel vikikusanyika karibu na maeneo yaliyojengwa.

    Umoja wa Mataifa pia ulionya kwamba chakula na mafuta yanaisha kwa zaidi ya milioni moja ambao bado wanajificha katika jiji hilo, kwa sababu haikuwa ikipokea msaada kupitia vivuko vya karibu.

    Soma zaidi:

    Mashambulizi ya Rafah: Ni nini kinachoendelea?

    Katika Picha: Wapalestina wakimbia baada ya Israel kushambulia Rafah