Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Tamaduni na Mambo Kale: Injili ya Imani na Matumaini - | Vatican News

Tafuta

2024.05.17 Partecipanti alla Plenaria della Pontificia Commissione di Archeologia

Tume ya Kipapa Kwa Ajili ya Tamaduni na Mambo Kale: Injili ya Imani na Matumaini

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amegusia kuhusu siku ya makatombe, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo; matumaini yanayobubujika kutoka katika Makatakombe; Ushuhuda wa wafia dini na waungama imani na kwamba, makatakombe ni amari za kidini na kwamba, anawapongeza kwa huduma hii makini ambayo inakita mizizi yake kwenye msingi wa imani. Makatakombe ni mahali pa sala, tafakari na ushuhuda wa imani na matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Benedikto XVI, kunako tarehe 30 Julai 2012 alitia saini kwenye hati ijulikanayo kwa lugha ya Kilatini “Pulchritudinis Fidei” iliyounganisha Tume ya Kipapa ya Utamaduni na Mambo ya Kale pamoja na Baraza la Kipapa la Utamaduni ambalo kwa sasa ni Baraza la Utamaduni na Elimu. Kuundwa kwa Tume hii ya Kipapa yalikuwa ni matunda na changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika ile Hati ya Kichungaji inayozungumzia Kanisa Ulimwenguni, “Gaudium et spes.” Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili wakati wa uongozi wake, aliunda Taasisi mbili ambazo kimsingi zilipewa jukumu la kuendeleza majadiliano ya kina na tamaduni pamoja na sanaa zinazofumbata utajiri wa imani na maisha ya Kikristo. Baraza la Kipapa la Utamaduni, likaundwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili kunako tarehe 20 Mei 1982 na hivyo kulitenganisha na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini lililopewa dhamana ya kukoleza mchakato wa majadiliano ya kidini na wale wasioamini. Tume ya Kipapa kwa ajili ya Utamaduni na Mambo ya Kale iliundwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili kunako tarehe 25 Machi 1993. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1952 Papa Pio wa Saba alikuwa ameunda Tume kuu ya Sanaa Takatifu.

Tume ya Kipapa ya Utamaduni na Mambo Kale
Tume ya Kipapa ya Utamaduni na Mambo Kale

Tume ya Kipapa kwa ajili ya Mambo ya Kale tangu mwaka 2007 hadi mwaka 2022 ilikuwa chini ya uongozi wa Kardinali Franco Ravas na kwa sasa iko chini ya uongozi na usimamizi wa Monsinyo Pasquale Iacobone, ambaye kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Utamaduni na Mambo Kale na kwamba, Tume hii kimsingi inaendelea kujipambanua kwa kuhakikisha kwamba, inawashirikisha vijana wa kizazi kipya katika tafiti za kina na bora zaidi; ili kukuza na kudumisha ubora wa tafiti zenyewe, ukarabati pamoja na kuthaminisha makatakombe ya Kikristo nchini Italia. Wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Utamaduni na Mambo Kale, Ijumaa tarehe 17 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, amegusia kuhusu siku ya makatombe, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo; matumaini yanayobubujika kutoka katika Makatakombe; Ushuhuda wa wafia dini na waungama imani na kwamba, makatakombe ni amari za kidini na kwamba, anawapongeza kwa huduma hii makini ambayo inakita mizizi yake kwenye msingi wa imani. Baba Mtakatifu anaipongeza Tume hii ya Kipapa kwa kuratibu na kuhamasisha Siku ya Makatakombe Duniani ambayo kwa kushirikiana na vyombo vya mawasiliano ya kijamii imesaidia sana kuragibisha na kutangaza makatakombe, kwa kushirikiana na vyombo vya mawasiliano na mitandao ya jamii; vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya huu kufanya na kuchapisha tafiti; pamoja na kuitisha makongamano na mikutano ya kimataifa.

Makatakombe ni mahali pa sala, ibada; imani na matumaini.
Makatakombe ni mahali pa sala, ibada; imani na matumaini.

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini”, kumbe makatakombe yatachukua uzito wa pekee katika maadhimisho haya, kama sehemu ya kumbukumbu ya utume na maisha ya watakatifu na kwamba, Makatakombe haya ni kielelezo cha matumaini ya maisha ya Kikristo baada ya mateso na kifo kazi ya Mungu inayotendwa na Kristo Yesu, Mchungaji mwema, anayewaalika waamini kwenda kushiriki utukufu wa mbinguni. Makatakombe haya ni makaburi ya Wakristo, kumbe huu ni ushuhuda wa ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Huku ni mahali ambapo waamini wa Kanisa la Mwanzo, walikuwa wanakutanika kusali na kuwaombea ndugu, na jamaa zao amani katika Kristo Yesu na Amani kwa Mungu wao! Baba Mtakatifu anasema, Maadhimisho ya mwaka 2025, kutakuwepo pia na Maadhimisho ya Makatakombe, Makaburi ya Mashuhuda na waungama imani. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kusali na kuwaombea Wakristo sehemu mbalimbali za dunia wanaodhulumiwa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo Yes una Kanisa lake. Tume hii ya Kipapa kwa niaba ya Kanisa zima na Vatican katika ujumla wake inatunza amana ya imani, sanaa na utajiri wa makatakombe ya Kikristo sehemu mbalimbali za Italia. Hii ni huduma inayokita mizizi yake katika mchakato wa uinjilishaji; huu ni ujumbe wa matumaini ya Kikristo sanjari na mang’amuzi ya imani.

Tume Mambo Kale
17 May 2024, 14:55